Utafiti wa ‘TWAWEZA’ umeonesha CCM ina nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi 2015

Utafiti uliofanywa na taasisi ya utafiti ya TWAWEZA umeonesha kuwa endapo uchaguzi ungefanyika mwezi mmoja uliopita, mgombea urais wa CCM John Magufuli angepata ushindi kwa asilimia 65.

untitled copy

Utafiti uliofanywa na taasisi ya utafiti ya TWAWEZA umeonesha kuwa endapo uchaguzi ungefanyika mwezi mmoja uliopita, mgombea urais wa CCM John Magufuli angepata ushindi kwa asilimia 65 wakati mgombea urais wa CHADEMA Edward Lowassa angefuatia kwa kupata asilimia 25.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa leo jijini Dar es salaam ambapo yameonesha pia kuwa wagombea wa CCM katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na ubunge na udiwani CCM inaongoza.

Katika ngazi ya udiwani CCM imeongoza kwa asilimia 60 ikifuatiwa na CHADEMA asilimia 24 na ngazi ya ubunge CCM imeongoza kwa asilimia 60 ikifuatiwa na CHADEMA yenye asilimia 26, wakatika katika ngazi ya urais bila kujali mgombea, CCM imeongoza kwa asilimia 66 ikifuatiwa na CHADEMA asilimia 22.

“Aidha, walipoulizwa watawachagua wagombea wa chama gani – bila kutajiwa majina ya wagombea – wananchi 6 kati ya 10 walisema kwamba watawachagua wagombea wa CCM kwa Urais, Ubunge (60%) na Udiwani (60%). Takwimu hizi zinatoa picha kwamba CCM inaungwa mkono, kama ilivyokuwa mwaka 2012.” Imesema taarifa iliyotolewa na TWAWEZA.

Akitangaza matokeo hayo mkurugenzi wa TWAWEZA bwana Aidan Eyakuze amesema utafiti huo ulifanyika mwishoni mwa mwezi Agost mwaka huu, na ulifanyika kwa njia ya simu kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa yote ya Tanzania.

Eyakuze amesema kuwa wananchi waliulizwa swali kuwa watamchagua nani bila kutajiwa majina na walipoombwa kutaja moja kwa moja jina la mgombea Urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea wa CCM, John Magufuli.

Amesema asilimia 25 walimtaja mgombea wa Chadema (na Ukawa), Edward Lowassa. Asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya wale waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea waliyempendelea.

Hata hivyo, takwimu zilikusanywa kabla vyama vingine, kikiwemo ACT-Wazalendo, kuteua wagombea wao wa Urais.

Amesema asilimia 62 ya wananchi wamesema kwamba wanajisikia wapo karibu zaidi na chama cha CCM kuliko vyama vingine.

Taarifa hiyo imeongeza pia kuwa “Chadema ni chama cha pili kinachopendwa kushinda vyama vingine vya upinzani. Lakini wananchi wanaosema kwamba watawachagua wagombea wa Chadema kwa Urais, Ubunge na Udiwani wamepungua kidogo. Ikumbukwe kuwa, inawezekana wananchi wanaopenda zaidi mseto wa Ukawa waliunga mkono vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi au NLD”.

Taarifa hiyo imeongeza pia kuwa mbali ya CCM na vyama vinavyounda UKAWA, chama cha ACT-Wazalendo kilitajwa na zaidi ya asilimia moja ya wananchi.

Utafiti huo ambao umetokana na kuwahoji watu 1848 umeonesha kuwa mgombea wa CCM, Dkt John Magufuli anapendwa zaidi na wanawake kuliko wanaume tofauti na Edward Lowassa, lakini pia wengi waliosema watamchagua Edward Lowassa ni wanaume na wengi wao ni walioelimika (wenye elimu kuanzia sekondari.

Waliomtaja Magufuli, wengi wao walisema wanamtaka Magufuli kwa sababu ni mchapakazi na waliomtaja Lowassa wengi wao wamesema ni kwa sababu wanaamini Lowassa ataleta mabadiliko.

Sehemu ya taarifa ya TWAWEZA inasema:-

“Hata hivyo, katika makundi yote haya, John Magufuli wa CCM anaonekana kuongoza. Kwa mfano, asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50. Pamoja na hayo, asilimia 57 ya watu wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 76 ya watu wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Magufuli. Upande wa makazi, asilimia 28 ya wakazi wa mijini walimuunga mkono Edward Lowassa tofauti na asilimia 24 ya wakazi wa vijijini. Asilimia 66 ya wakazi wa vijijini na asilimia 61 ya wakazi wa mijini wanamuunga mkono John Magufuli.

Asilimia 26 ya wanaomuunga mkono John Magufuli walidai kwamba ni kwasababu yeye ni mchapakazi, na asilimia 12 ya wanaomuunga mkono Edward Lowassa walisisitiza kwamba anaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini. Izingatiwe kwamba kauli hizi zinafanana karibu neno kwa neno na kauli mbiu za kampeni za wagombea hawa wawili.

Hata hivyo, wananchi hawana taarifa sahihi juu ya nafasi rasmi ya Ukawa kama mseto. Asilimia 49 ya wananchi wanafikiri kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa, kinyume na hali halisi. Asilimia 57 wanafikiri kwamba neno ‘Ukawa’ litakuwepo kwenye karatasi zao za kupigia kura. Hii pia, sio kweli. Bila kampeni na juhudi za kuwaelimisha wapiga kura ili wawe na taarifa sahihi kuhusu jambo hili, hali hii inaweza kuleta wasiwasi siku ya uchaguzi.”

Advertisements

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s